Ni kweli, matukio ya kutisha kwa kipindi
hiki yamekuwa sehemu ya maisha yangu, lakini sasa naona kama yamezidi!
Moyoni niliogopa sana.
Nilichanganyikiwa zaidi hasa kwa kuwa
nilikuwa nina uhakika kwamba mlango niliufunga kabla sijalala. Mzee huyu
anaendelea kunikazia macho.
Ghafla anaanza kuangua kicheko kikali, halafu
anapiga hatua za taratibu kutoka pale mlangoni aliposimama na kunisogelea
kitandani!
“Wewe ni nani?” nikamwuliza kwa ukali,
nikijaribu kumtisha.
Hakujibu, akaendelea kunifuata, kicheko
kikimtawala. Kilikuwa kicheko kikali ambacho nilikuwa nina uhakika kwamba
majirani zangu walikuwa wakikisikia, lakini hakuna aliyeamka.
Ni saa 8:45 usiku!
Bado maswali mengi kichwani yalinitawala
juu ya mzee huyu ambaye haeleweki. Mapigo ya moyo wangu yaliongezeka kasi.
Nikabaki natetemeka kwa woga. Kuna kitu kiliniingia akilini mwangu kwa kasi ya
ajabu sana.
Nilitakiwa kufanya jambo fulani ili kuniepusha
na hatari ambayo ilikuwa mbele yangu. Baada ya ukimya wangu wa muda mrefu kuona
kwamba hausaidii kitu, nilipata wazo jipya. Nilitakiwa kuwa mkali kidogo kwa
mzee huyu.
“Tokaaaaa...” nikapiga kelele.
Hakuondoka, akaendelea kunisogelea.
“Nimekwambia tokaaaa...” nikazidi kupaza
sauti lakini haikusaidia kitu.
Kitendo cha kumwambia atoke ni kama
nilimwambia aendelee kunifuata. Akazidisha hatua zake za kunifuata pale
kitandani. Alipofika usawa wa kitanda kabisa, hatua kama tatu ili anifikie,
akasimama.
Hakusema chochote!
Nikazidi kuogopa.
“Nani wewe?” nikamwuliza kwa sauti kubwa
kabisa.
“Nani wewe?” naye akaniuliza badala ya
kujibu.
“Nimekuuliza nani wewe?”
“Hebu tulia wewe...” akasema kwa sauti ya
ukali.
“Nitulie?”
“Tulia.”
“Kwani umekuja kwangu kufanya nini?”
“Unataka kujua?”
“Ndiyo!”
“Basi unyamaze, unachotakiwa kufanya ni
kunisikiliza kwa kila kitu nitakachokuambia,” akaniambia akionekana kuwa na
hasira sana.
“Sawa nanyamaza...” nikamjibu.
Alinyoosha mkono wake
mmoja juu, nikashangaa kuona unazidi kwenda hewani. Nikakaza macho, mkono
ukazidi kupaa juu. Ulikua taratibu hadi ukatoboa dari.
“Mamaaa...” nikapiga
kelele.
“Lakini nilikuambia
usipige kelele.”
“Wewe ni nani?”
“Unadhani naweza kuwa
nani?”
“Jini!”
Nilipotamka maneno hayo
akatoweka na kuniacha peke yangu. Nikabaki najiuliza maswali ambayo hayakuwa na
majibu. Nikiwa katika hali hiyo, nikashtuka sana! Nilikuwa chumbani mwangu
nimelala.
Kwa maneno rahisi,
nilikuwa naota. Hata hivyo ni ndoto ambayo hunichanganya kila wakati. Ndoto za
kutisha zimekuwa sehemu ya maisha yangu!
Siyo siri nilijichukia!
Mwili wangu ulitetemeka,
nikihema kwa kasi sana. Nilikurupuka kitandani kisha nikalifuata dirisha na
kufungua pazia kuangalia nje. Niliona giza. Kwamba bado kulikuwa hakujapambazuka.
Nikarudi kitandani na
kunyoosha miguu yangu, huku nikiwa nimekaa kwa kuegemea mto upande wa juu.
Nilianza kuitafakari ndoto ile bila kupata majibu. Nikapata wazo la kuangalia
saa iliyokuwa ukutani!
Nilishtuka sana.
Ilionesha ni saa 8:45 usiku!
Nilitamani ardhi ipasuke niingie ndani
yake. Wakati tukio lile likitokea kwenye ndoto, saa niliyoiona ilionesha saa
8:45, sawa na hii ninayoitazama ukutani sasa hivi. Kwa kweli nilichanganyikiwa
sana, nikahisi kuzimia.
“Ina maana muda huu ndiyo nilikuwa katika
tukio lile? Hapana, lazima nifanye kitu. Naweza kufa hivi hivi nikijiona...”
nikawaza kichwani mwangu.
“...na kweli unaweza kufa hivyo hivyo...”
nikasikia sauti hii kama mwangwi ikitamka.
Nikatetemeka.
USIPITWE NA KILICHOENDELEA............
No comments:
Post a Comment