![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjX4Q1wnQSHSb8gN4LvpQjpb0EzXil0KwPBayx274-lop74ZX500auWp_hZ_kwOoYUYQxCmDp6oERgVkJrTdlI39A3WhWSEse0dvUUJGRoBRtr00PxlWMOVKhWh2JSU_0vOc22QX3plDBZl/s320/IMG-20150429-WA0077.jpg)
Sehemu ya Maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania wakiongoza shughuli ya kuusafirisha mwili wa Marehemu Brigedia Jenerali(Mstaafu) Hashim Mbita kuelekea kwenye nyumba yake ya milele, Makaburi ya Kisutu, Jijini Dar es Salaam
Rais
Kikwete alipokea taarifa hiyo ya msiba alipoingia tu Uwanja wa Uhuru,
Dar es Salaam, kuongoza maelfu ya wananchi kuadhimisha miaka 51 ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, aliuelezea msiba huo kama msiba wa
simanzi kubwa.
“Ni
wachache katika nchi yetu wanaoweza kulinganishwa na Mzee Hashim Mbita
kwa kiwango cha utumishi uliotukuka, wa miaka mingi na usiokuwa na
kasoro. Katika utumishi wa Serikali alipata kuwa Mwandishi wa Habari
Mkuu wa Idara ya Habari na pia kuwa Mwandishi wa Habari wa Rais kabla na
baadaye kuwa Balozi wa Tanzania katika Zimbabwe. Kazi zote alizifanya
kwa ufanisi mkubwa sana,”alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katika
Chama cha TANU alikuwa Katibu Mtendaji wa Chama na katika Jeshi letu
makini, Mzee Mbita alipata na kufikia cheo cha Brigedia Jenerali, yote
mambo makubwa kweli kweli.
“Lakini
ilikuwa katika nafasi ya Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya Umoja
wa Afrika ambako Mzee Mbita alikamilisha utumishi wake kwa kusimamia
shughuli nzito ya kuwasaidia ndugu zetu Kusini mwa Afrika kwa miaka 20
mfululizo, miongo miwili, na kuweza kupata uhuru wao. Hakuna mpigania
uhuru katika Msumbiji, Zimbabwe, Namibia, Angola na hatimaye katika
Afrika Kusini ukiondoa nchi nyingine kama Cape Verde, asiyejua mchango
wa Mzee Mbita.
Wote
hawa amewatumia vizuri, kwa ufanisi, kama mlezi, kama kiongozi, kama
kamanda hadi wakafanikisha kazi ya ukombozi. Huu ni mchango mkubwa kweli
kweli.
“Kitendo
chake cha mwisho cha utumishi, kilikuwa kuongoza shughuli za Mradi wa
Hashim Mbita wa Kuweka Kumbukumbu za Harakati za Ukombozi Kusini mwa
Afrika na Kuenzi Viongozi Wakuu (Hashim Mbita Project to Honour
Outstanding Leaders), kazi ambayo nayo aliifanya kwa uwezo na ufanisi
mkubwa na ripoti yake tukaizindua mwaka jana pale Victoria Falls,
Zimbabwe wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),”alisema Rais Kikwete.
Alisema
Zimbabwe ilitangaza kumpa Mzee Mbita Nishani ya The Royal Order
Munhumutapa yenye kutambua mchango wake katika harakati za ukombozi wa
Zimbabwe. Mzee
Mbita amekuwa raia wa sita wa kigeni, na wa kwanza asiyekuwa rais,
kupata heshima hiyo ya juu kabisa ambayo hutolewa na Taifa la Zimbabwe
kwa wageni ambao wamechangia Uhuru wa Zimbabwe.
Viongozi
watano wa mwanzo kupata Nishani hiyo, mwaka 2005, walikuwa ni Marais na
Viongozi Waanzilishi wa Kundi la Nchi za Frontline States dhidi ya
Ukoloni na Ubaguzi wa Rangi, Marehemu Julius Kambarage Nyerere, Mzee
Kenneth David Kaunda wa Zambia, Marehemu Sir Seretse Khama wa Botswana,
Marehemu Samora Moises Machel wa Musumbiji na Marehemu Augustinho Neto
wa Angola.
Brigedia
Jenerali mstaafu, Hashim Mbita amefariki dunia katika Hospitali ya Kuu
ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo, Dare es
Salaam. Mbita
ambaye alikuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya uliokuwa Umoja
wa Nchi Huru za Afrika (OAU), alifariki dunia leo majira ya saa 3
asubuhi.
Akizungumza nyumbani kwa
marehemu Chang’ombe, Temeke, mtoto wa marehemu, Iddi Mbita amesema baba
yake alifariki kutoka na kusumbuliwa na shinikizo la damu,
“Mzee alikuwa
anasumbuliwa na shinikizo la damu na leo (jana) ameamka salama, akanywa
chai na dawa, kisha akaomba kupumzika. Baada ya muda mfupi akafariki
dunia asubuhi muda saa 3,” alisema Iddi.
Alisema marehemu Mbita
alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la hilo tangu Agosti mwaka jana, hivyo
kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema akiwa katika hospitali hiyo, aliwekwa chini ya Uangalizi Maalum wa Daktari (ICU).
Alisema alikaa katika
hospitali hiyo kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu na ilipofika Oktoba
mwaka jana alipelekwa nchini India kwa matibabu zaidi.
Iddi alisema alikaa
nchini India kwa miezi miwili na Januari mwaka huu alirudishwa nchini na
kuendelea na matibabu nyumbani kwake Chang’ombe jirani na Klabu ya TCC
Chang’ombe.
Alisema kwamba Machi 23
mwaka huu Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania JWTZ walimfuata na
kumchukua kwa ajili ya kumpatia matibabu zaidi.
Alisema baada ya vipimo
mdaktari katika Hospitali ya Lugalo walibaini kuwa kuna matatizo
mbalimbali yaliyokuwa yakimsibu hivyo aliendelea kupata matibabu hadi
alipoaga dunia.
“Unajua ugonjwa ulikuwa
umemla sana hivyo kusababisha organ (mfumo wa viungo vya mwili)
mbalimbali kupata hitilafu,” alisema Iddi.
No comments:
Post a Comment