ASKARI wawili wa Jeshi la Polisi katika Kituo cha Ikwiriri wilayani
Rufiji mkoani Pwani, wameuawa baada ya kushambuliwa kwa silaha na
majambazi, waliovamia kituo hicho na kuiba silaha baada ya kufanikisha
mauaji.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi liko katika msako mkali, huku
Mkuu wa jeshi hilo, IGP, Ernest Mangu akitangaza donge nono la Sh
milioni 20 kwa watakaofanikisha kukamatwa kwa wahusika wa tukio hilo na
silaha.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu kutoka eneo la
tukio, Ikwiriri, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei alisema
majambazi hao walitumia silaha kuwaua askari hao.
Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 8 usiku
katika kituo hicho cha Polisi cha Ikwiriri.
Aliwataja askari waliokufa
kuwa ni mwenye namba E 8732 Koplo Edgar Milinga na WP 5558 Konstebo
Judith Timothy.
Alisema licha ya kufanya mauaji hayo, pia majambazi hao yalipora
silaha tano za moto aina mbalimbali, zikiwemo SMG 2, SAR 3 na risasi 60.
Pia, walichukua mabomu mawili ya machozi.
Kamanda alisema kuwa pia watu hao, waliharibu kwa kulipiga risasi gari la Polisi la kituo hicho lenye namba za usajili PT 1965.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba alisema tukio hilo
la kusikitisha, halitapita hivi hivi, bali jeshi limeelekeza nguvu zake
huko kuhakikisha wahusika wanakamatwa.

No comments:
Post a Comment